Tuesday, January 21, 2014

Pata Historia ya Wilaya ya Korogwe Hapa

Historia ya Wilaya ya Korogwe

Wilaya ya Korogwe ilianza mwaka 1966  ambapo ilitenganishwa na Wilaya ya Lushoto. Kutokana na Wilaya ya Lushoto kuwa na eneo kubwa kiutawala, ilikuwa vigumu kutoa huduma kwa wananchi. Kabla eneo hili halijatengana na Wilaya ya Lushoto lilijulikana kama Korogwe “Sub-District” na mtawala wa eneo alikuwa ni “District Officer Incharge”.

Asili ya jina Korogwe ni jina la mmoja wa wakazi wa awali wa eneo hilo ambaye alijulikana kama Mkorogwe ambaye alikuwa ni Mzigua kwa kabila aliyeishi katika kitongoji cha Kilole- Kambi  ya  Maziwa.  Mwaka 1966  Korogwe ilitangazwa kuwa Wilaya kupitia Tangazo la Serikali Na. 429 la Mwaka 1966 (GN No.429 of 1966). Mkuu wa Wilaya wa kwanza aliitwa Rajabu Semvua, wakati huo ilikuwa na Tarafa nne (4) ambazo ni Korogwe, Mombo, Bungu na Magoma kwa kuzingatia mfumo wa Kichifu uliokuwepo kabla ya Uhuru.

Kufuatia Tangazo hilo la Serikali ilianzishwa Halmashauri kamili iliyojulikana kama Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. Mtendaji Mkuu wa Halmashauri kwa wakati  huo alijulikana kama Mkurugenzi  wa Maendeleo wa  Wilaya (District  Development  Director- DDD) ambaye alishirikiana na Wakuu wa Idara mbalimbali katika kufanikisha utendaji kazi wa Ofisi yake. Katika  jitahada za kusogeza huduma karibu na wananchi, Serikali kupitia Tangazo Na. 352 la tarehe 19/7/2004 ilianzisha Halmashauri ya Mji na kuifanya Wilaya ya

Korogwe kuwa na Halmashauri mbili (Halmashauri ya Mji na Wilaya). Wilaya ina eneo lenye kilomita za mraba 3,756 ambazo zimegawanyika katika Halmashauri ya Mji Korogwe yenye Kilomita za mraba 212 na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe yenye Kilomita 3,544. Halmashauri  hizi  zina  Tarafa  5, Kata 28, Vijiji  139, Vitongoji  610 na Mitaa 17  na zinakadiriwa kuwa na jumla ya watu 324,020.

Wilaya ya Korogwe inapitiwa na barabara kuu inayoiunganisha na Miji mikubwa ya Dar-es- salaam,  Arusha, Kilimanjaro, Pwani, Tanga Mjini, Morogoro na nchi za jirani ambazo ni Kenya na Uganda, hii inaifanya Korogwe kuwa Mji wa Kibiashara.

 


No comments:

Post a Comment